Tafakari na mahubiri ya leo tunaangalia ujumbe huu mzito juu ya ushindi wa Mungu dhidi ya miungu mingine, na umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi katika utumishi wako kwa Bwana.
Wapo wengi ambao bado wana wasiwasi na Mungu wa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo. Mungu ambaye wamemchagua na kumwamini. Japo wameamini, bado wana mashaka na imani zao, na bado wanategemea miungu mingine. Kwa kupitia Biblia ninataka kukuonyesha ni kwa jinsi gani Mungu wa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo, Mungu wa Biblia aliyetenda na anaye endelea kutenda matendo makuu tayari amekwisha kuwashinda hao miungu mingine ambayo wewe unaiamini na kuitegemea. Tuliangazie neno la Mungu kwa kina hapa…
Japo kuna ambao wanaweza wasiamini kuwa kuna miungu mingine, Biblia inatuambia fika kabisa kuwa kuna miungu mingine mingi. Kuna miungu ya kidini na miungu ya makabila ambayo wanadamu wanaitumikia. Wakristo walioamini katika kanisa la kristo ni miongoni mwa watu ambao bado wanafungamana na imani za miungu mingine. Kuna ambao pamoja na kuipokea imani katika Kristo Yesu bado wanafungamana na kuiamini miungu na imani za kale. Bado hawajafanya maamuzi sahihi katika imani zao. Leo ninataka kukudhibitishia kuwa hao miungu na imani unazofungamana nazo kwa Kristo tayari zilishashindwa na hazina nguvu tena. Hauna haja ya kuukosa ufalme wa Mungu wa mbinguni kwa kuendelea kufungamana na hiyo miungu na imani zake. Katika Kristo uliwekwa huru na mbali na hao miungu na imani nyinginezo.
Tafakari ushindi huu ambao Mungu anatuonyesha katika neno lake…
Kutoka 12:12 – Mungu hakuwashinda tu Wamisri, bali aliwashinda pia miungu wa Misri na kujihidhirisha kwao kuwa yeye ndiye Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana. Misri ilikua na miungu yake, lakini Mungu alijiinulia utukufu kwa kuishinda miungu ya wamisri na kuwadhibitishia kuwa yeye ndiye Mungu wa kweli. Miungu wa babu zako tayari walishashindwa na hawana mamlaka juu yako tena.
1 Sam 5:1-5 – Mungu aliweka vita na wafilisti na kuwashinda pamoja na Mungu wao Dagoni. Mungu wa Mbinguni hawezi kulinganishwa na miungu mingine kamwe. Usimlinganishe Mungu wa Mbinguni na miungu yako. Yeye atabaki kuwa Mungu wa miungu. Mungu hawezi kugawana utukufu wake na miungu mingine. Ukimlinganisha na miungu mingine yeye atainuka mshindi dhidi yao.
Isaya 21:9 – Mungu aliwashinda wababiloni pamoja na miungu yao. Pamoja na hao miungu unayoitegemea, tambua kuwa Mungu ndiye mwenye mamlaka juu yao wote. Hakuna atakayeweza kumshinda Mungu wetu wa mbinguni.
Mathayo 12:28-29 – Yesu alitukomboa na kutuweka huru dhidi ya yule mwovu kwa damu yake ya dhamani. Je ni mapepo au roho za kuzimu zinakusumbua na kukusababisha kuitafuta miungu mingine? Yesu kwa damu yake ya thamani iliyomwagika pale msalabani alishatukomboa na haya yote. Yesu alishatuweka huru kweli kweli. Na amini usiamini hakuna atakayeweza kututenga na upendo wake kamwe (Rum 8:35-39).
Zaburi 86:8 – Hakuna Mungu mwingine awezaye kufanya yale ayafanyayo Mungu wetu wa Mbinguni. Hao miungu na imani nyinginezo ni maigizo kwake. Hao wanafanya tu mazingambwe.
Zaburi 96:4 – Mungu tumwaminiye ni Mungu mkuu zaidi ya miungu mingine yote ile. Anastahili kuheshimiwa na kuabudiwa, hatogawana utukufu wake na miungu mingine yeyote.
Mungu bado anaendelea kupokea sifa za kuwa Mungu Mkuu katika zaburi 95:3, 97:7, 135:5.
Na zaidi ya yote, bado leo tunaendelea kushuhudia ushindi wa Mungu dhidi ya miungi mingine katika ulimwengu wa leo. Mapepo yanatoka kwa jina la Yesu Kristo, watu wanaendelea kupokea uponyaji na kufunguliwa, watu wanaendelea kuokolewa na kuingia katika ufalme wa Mungu siku hadi siku. Je, ni Mungu yupi yule ambaye wewe umechagua kumwamini na kumtumikia? Ni Mungu ambaye ameendelea kushinda vita vya kila aina au ni miungu inayoendelea kushindwa? Je, wewe unataka kufanana na hao ambao walikua na miungu yao iliyoshindwa? Biblia inasema ‘ amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu na kumfanya kinga yake’ (Yer 17:5). Pia inasema ‘ Amtegemeaye Mungu ni kama mlima Sayuni, hatotikisika kamwe’ (Zab 125:1) Mimi na nyumba yangu tumechagua kumtumikia Bwana (Yoshua 24:15) wa majeshi aliyetushindia na atakaye endelea kutushindia. Yoshua anajaribu kutufundisha leo kwamba waweza kuamua ni yupi utakaye mtumikia katika maisha yako awe Mungu kwako. Maamuzi yamewekwa mikononi mwako kumtumikia Mungu ambaye ndiye BWANA au kumtumikia mungu ambaye ni mungu baali. Lakini ni lazima utambue kuwa hakuna awezaye kuwatumikia mabwana wawili (Mat 6:24), ni lazima uchague ni yupi utakayemtumikia. Mungu wa mbinguni hataki kuchanganywa na miungu wengine.
Hatua gani uchukue?
Kumbukumbu la Torati 32:17, “Walitoa sadaka kwa pepo, si Mungu, Kwa miungu wasiyoijua, Kwa miungu mipya iliyotokea siku zilizo karibu, Ambayo baba zenu hawakuiogopa.” Kupitia neno la Mungu wewe tayari umeshamjua Mungu wa kweli ni yupi.
Hivyo basi, achana na hao miungu wako wa ziada na amini tu katika Mungu wa kweli ambaye yeye anaweza kuteketeza mwili na roho jehanamu (Matayo 10:28, Kumb 8:19), vitu ambavyo shetani pamoja na vitisho vyake vyote, na miungu yake yote hawezi kuteketeza. Weka imani yako kwa Mungu ambaye ana nguvu na mamlaka juu ya hivyo vimiungu vidogo unavyovitegemea na kuviamini. Amini katika Kristo ambaye kwa njia ya msalaba tayari amekwisha kukupatia ushindi, uhuru, na wokovu wa milele katika yote yale unayopitia (Wakolosai 2:15, Waefeso 8:4). Yesu tayari amekwisha kutuweka huru. Amini katika Mungu wa ushindi na ubaki kuwa mshindi.
Katika kinywa chako pasiwepo na miungu mingine (kutoka 23:13), usifanye ibada wala kuabudu miungu mingine (kutoka 34:14, kumb 6:14), tena kaa mbali na jitenge nao washirikio katika ibada za miungu mingine (kumb 6:14, 1 Korintho 8:4), usiwe na miungu mingine zaidi ya Mungu (kutoka 20:3, Isaya 44:6), kwani hakuna Mungu zaidi yake (Kumb 4:35, Isaya 45:5, Isaiah 43:10) na zaidi ya yote usiibadili kweli ya Mungu (Rum 1:25) wala usiamini katika kila roho (1 Yoh 4:1).
Ushindi wa Kristo ni wa milele na atatawala milele (Luka 1:32-33), utawala na ushindi wake hauna kikomo (Ufunuo 11:15). Shetani na miungu yake haina nguvu dhidi ya Kristo Yesu Bwana wetu. Kwa wale wamwaminio amewatia mafuta na muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu (Korintho 1:22, waefeso 1:14).
Ufalme wa Mungu sio wa maneno bali wa nguvu na ushindi. Kuza imani yako ndani ya Kristo kwa Mungu wa kweli kwani imani yetu sio ya kutetemeshwa (Waebrania 12:28), kwani wenye utajiri wa imani katika yeye ndio watakao urithi ufalme wa Mungu (Yakobo 2:5).
Nikutakie kila la kheri na baraka tele katika kuchagua lile lililo sahihi katika ufalme wa Mungu. Kama una swali ama maoni juu ya hili usisite kunishirikisha. Ahsante kwa kusoma, na Mungu akubariki na aendelee kukuimarisha.
Kwasababu ya Kalvari mimi nimewekwa Huru,
Rumishael Ulomi (BD,BCL,MA)
