Je unayafahamu maagano ambayo
Mungu alifanya na watu wake na maana yake? Kama bado, basi waweza kujifunza
hapa kwenye makala ya leo. Pia waweza kushare na mwenzako ili naye aweze
kujifunza zaidi juu ya maagano haya ambayo Mungu alifanya na wanadamu ili kuendeleza,
kuratibisha, kusimamia, na kueneza ufalme wake toka Mbinguni hadi duniani alipo
mwanadamu aliyemuumba kwa mfano wake. Pale tunaposali sala ya Baba yetu wa
mbinguni kwa kusema ‘Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe duniani kama huko Mbinguni’ huu ndio ufalme wa Mungu tunao uzungumzia. Mungu kupitia maagano yake
na mwanadamu alikua akisimamia na kueneza ufalme wake hapa duniani. Katika
maagano haya tumajifunza ushirikiano wa Mungu na mwanadamu katika usimamizi na utawala
wa ufalme wake.
Ni ngumu sana kuwakuta
wakristo katika ulimwengu wa sasa wakizungunza kuhusu maagano. Lakini ukweli ni
kwamba, sisi kama wakristo katika kanisa la Kristo yatupasa kukumbuka na
kuyajadili maagano haya ambayo Mungu alifanya na wanadamu. Maagano ni mojawapo
ya mada muhimu sana katika Biblia kwani ndio msingi wa kuelewa zaidi hadithi
nzima ya ukombozi katika Biblia. Ukombozi wetu kwa Kristo umejengwa katika
msingi wa maagano haya.
Tukitazama kuanzia kitabu cha
Mwanzo katika Biblia na kuendelea, tunaona Mungu akiingia katika uhusiano mmoja
baada ya mwingine (yaani, maagano) na wanadamu mbalimbali ili kuokoa ulimwengu
wake na kuendeleza ufalme wake duniani.
Maagano ya Mungu katika Biblia
Kuna maagano mengi katika
Biblia, lakini katika makala hii tutaangazi maagano matano muhimu kwetu ambayo
yanatusaidia katika kuelewa hadithi ya Biblia na mpango wa Mungu katika kuleta
ukombozi kwa mwanadamu aliyepotea na kusimamia na kueneza ufalme wake duniani.
Maagano hayo ni: Agano na Adamu, Agano la Nuhu, Agano la Ibrahimu, Agano la
Musa, Agano la Daudi, na Agano Jipya. Lakini makala hii itaangalia zaidi
maagano yaliyopo katika agano la kale, kisha hapo baadae tutakua na makala ya
pili ambayo itaangazia kwa kina agano jipya.
Agano na Adamu – Agano la msingi
Agano lakwanza katika Biblia
ni Agano ambalo Mungu alifanya na Adamu (Mwanzo 1-3, Hosea 6:7), Hili lilikuwa
ni agano la msingi kwa mwanadamu na msingi wa maagano mengine yote yaliyofuata
baadaye. Agano hili lilitoa malengo ya Ufalme wa Mungu na wajibu na majukumu ya
mwanadamu katika ufalme wa Mungu hapa duniani kabla na baada ya mwanadamu
kutenda dhambi na kwenda kinyume na Mungu. Katika Agano na Adamu, mwanadamu
aliumbwa kwa mfano wa Mungu ili kuratibisha shughuli na kueneza ufalme wa Mungu
ulimwenguni kote (Mwanzo 1:27-28, 5:1-2).
Wanatheolojia wanaliita agano
hili ‘Agano la Mungu na Adamu’ kuwa ni agano la kazi kwa sababu linatokana na
kanuni ya utii wa Adamu. Wapo wachache ambao husema kuwa Mungu hakufanya Agano
na Adamu na hii ni kutokana na kuwa Mungu hapo mwanzo hakutumia neno ‘Agano’ katika
jambo lolote alilosema kuhusu Adamu. Lakini katika Hosea 6:7, tunaamini kuwa
Mungu alifanya Agano na Adamu. Kutokuwepo kwa neno "agano", katika kumbukumbu
za kibiblia hasa katika kitabu cha Mwanzo haimaanishi kwamba hakuna agano
lililokuwepo. Hata baada ya Adamu na Hawa kufukuzwa kutika katika bustani ya
Edeni, waliendelea kuwa chini ya agano hilo. Biblia inatuonyesha fika kuwa toka
uzawa wa Adamu na kuendelea Mungu aliendelea kufanya maagano na watu wake.
JIFUNZE ZAIDI JUU YA AGANO HILI 'KWA KUBOFYA HAPA'
Agano na Nuhu – Agano na viumbe wote, Ahadi ya
kutoharibiwa kwa ulimwengu
Agano la pili katika Biblia Mungu
alilifanya na Nuhu (Mwanzo 6:18;9:9-17), baada ya Gharika, Mungu alifanya agano
lingine na Nuhu, Agano la utulivu (stability). Hili linajulikana kama agano la
Nuhu. Ukisoma Mwanzo 9, hili ni agano ambalo Mungu anaweka na Nuhu baada ya
gharika ambapo anafanya upya kwa kudhibitisha baraka za uumbaji, sura ya Mungu ndani
ya mwanadamu na kazi ya kutawala nchi. Mungu anaingia katika uhusiano (Agano) na
Nuhu na viumbe vyote hai akiahidi kwamba licha ya uovu wa wanadamu
hatawaangamiza tena, kwamba hatoiangamiza tena dunia kwa maji (gharika) wala
kuilaani nchi, na kama ishara ya agano alilofanya na Nuhu, Mungu “akaweka
upinde wake mawinguni.
Pia Kama ilivyokuwa kwa agano lake na Adamu hapo awali, katika Agano hili Mungu alilifanya kwa upya Agano lake na Adamu kwa Nuhu. Nuhu na familia yake waliamriwa waijaze dunia. Kwa Agano hili Mungu aliahidi kutawala juu ya dunia kwa wanadamu na uzima wa milele kama malipo ya utii.
Agano la Nuhu lina sifa tatu
za msingi. Kwanza, ni agano lisilo na masharti, na hii ni kutokana na kwamba
halikutegemea chochote ambacho Nuhu au uzao wake ungefanya ili kulitimiza
agano. Pili, lilikua ni agano lililofanywa kwa Nuhu na uzao wake wote pamoja na
“kila kiumbe hai” na dunia nzima kwa ujumla (Mwanzo 9:8-10). Tatu, Agano hili
lilitiwa muhuri kwa ishara ya upinde wa mvua. Ahadi za agano hili zilitegemea
uaminifu wa Mungu peke yake na si vinginevyo. Hili ni Agano kati ya Mungu na
kila kiumbe duniani (Mwanzo 9:17).
Soma zaidi: Mwanzo sura ya 8:20-9:17
Agano na Ibrahamu – Ahadi na Kuzaliwa kwa Taifa la
Israeli
Agano la tatu ni Agano kati
ya na Abrahamu (Mwanzo 15,17). Katika Agano hili Mungu anamuahidi Ibrahimu
nchi, uzao na baraka. Agano hili ni agano la kuchaguliwa kwa Israel kuwa taifa
ambalo Mungu atalitumia katika kueneza na kuratibisha ufalme wake hapa duniani.
Katika agano hili Mungu aliahidi kuwa angembariki Ibrahimu kwa njia tatu. Sehemu
ya kwanza ya agano hili inajulikana kama nchi ya ahadi ya Kanaani (Mwanzo 12:1,
Mwanzo 15:7), ambapo Ibrahimu anaitwa na Mungu kutoka katika nchi ya baba zake
Uru na kwenda mahali panapojulikana kama Kanaani. Nchi ambayo baadaye
ilijulikana kama Israeli.
Ahadi ya pili ni kuwa Mungu
angemfanya kuwa taifa kubwa (Mwanzo 12:2 - Hapa ndipo Mungu alipoahidi kwamba
angefanya taifa kubwa kutoka kwake, na hapa ndipo Mungu alipobadilisha jina la
Abramu kuwa Ibrahimu likimaanisha ‘baba wa mataifa mengi) na hivyo kulifanya jina
lake kuwa kuu, na hatimaye baraka ya tatu ni kuwa kupitia yeye Mungu angebariki
mataifa mengine (Mwanzo 12:3).
Kama sehemu ya agano hili na
Ibrahimu, Mungu alimwambia Ibrahimu kuondoa govi lake na govi za wavulana wote
wa Kiyahudi baada yake. Utaratibu huu unajulikana kama tohara/kutairi na ni
ishara ya agano la Ibrahimu na Mungu. Kulielewa Agano hili ni muhimu sana katika
kuelewa dhana za kitheolojia kama vile Nchi ya Ahadi, uchaguzi wa wana wa
Israeli, watu wa Mungu, urithi na kadhalika. Kulielewa agano hili kunatoa
muktadha wa kuelewa zaidi desturi kama vile tohara, migogoro na mataifa yaliyowazunguka
na migawanyiko kati ya Wayahudi na mataifa mengine.
Soma zaidi: Mwanzo sura ya
12, 15, and 17
Agano na Musa – Mwanzo wa Sheria kwa watu wa
Mungu/Taifa la Israeli
Agano la Nne ni Agano kati ya
Mungu na Musa pamoja na wana wa Israeli. Agano hili linatambulika kama Agano la
Musa (lililoitwa baada ya Musa), ambalo pia linajulikana kama agano la Sinai
(linaloitwa baada ya Mlima Sinai wa Biblia), ni agano ambalo Mungu aliliweka na
wana wa Israeli kwenye Mlima Sinai baada ya kuwatoa utumwani Misri. Mungu
aliwakomboa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri na kuahidi kuwafanya kuwa
mali yake mwenyewe yenye kuthaminiwa, taifa takatifu, lililotengwa kwa ajili
yake, kwa kazi maalumu ya kueneza ufalme na utukufu wake ulimwenguni. Yeye
(Yahwe) atakuwa Mungu wao na wao (Israeli) watakuwa watu wake.
Walipokuwa wakitembea kutoka Bahari
ya Shamu hadi nyikani, Wana wa Israeli hawakujua ni nini walichotarajia, lakini
walipofika chini ya Mlima Sinai, waligundua kwamba Mungu alikuwa amechagua mahali
hapa ili kujidhihirisha kwao na kuingia katika agano nao.
Mungu alimchagua na kufanya
agano na Musa ( Kutoka 19-24) pamoja na wana wa Israeli. Musa na watu wake
walipofika Mlima Sinai baada ya kutoka Misri kuelekea Nchi ya Ahadi, Mungu
alizungumza na Musa. Hapa ndipo Mungu alipofanya agano na Musa na watu wake
ambalo lililifanya upya lile alilokuwa amefanya na Ibrahimu. Wakati huo huo,
Mungu aliwapa Amri Kumi – kanuni na sheria ambazo walipaswa kuishi nazo kama
taifa teule la Mungu. Sheria ambazo ziliwaunganisha wayahudi wote kuwa taifa
moja la Israeli. Sheria ambayo ilikusudia kuwatawala na kuwafanyiza watu wa
Israeli katika Nchi ya Ahadi. Sheria hii haikuwa njia ya wokovu bali iliwatenga
na kuwatofautisha na watu wengine wa mataifa yaliyowazunguka, hii ilikuwa ni
kuwafanya kuwa taifa pekee la makuhani wa Mungu (Kutoka 19:1-7) katika
kuendeleza ufalme wa Mungu hapa duniani. Agano hili lilikuwa na masharti na
lilifafanuwa baraka na laana ambazo wangepokea kulingana na utii au kutotii (Kumbukumbu
la Torati 28-29).
Agano ambalo Mungu alifanya
na Musa lilijengwa juu ya agano alilofanya na Ibrahimu, na kwa agano hili,
Mungu aliwaongoza wana wa Israeli kuielekea nchi yao ya ahadi.
Soma Zaidi: Kutoka Sura ya
19-24
Agano na Daudi – Agano la kifalme
Agano la tano na la Mwisho
kwa Makala ya leo ni Agano kati ya Mungu na Mfalme Daudi (nyumba/uzao wa
Daudi). Mungu alifanya agano na mfalme Daudi (Zaburi 89, 132). Agano lake na
Mfalme Daudi ni agano ambalo liliwafanya Daudi na uzao wake kuwa warithi wa
kifalme katika taifa la Israeli Daima (2 Sam. 7:12-13). Katika Agano hili kwa
kifupi ni kwamba Mungu anamweka Daudi kuwa mfalme juu ya Israeli na kuahidi
kufanya jina lake kuwa kuu. Anaahidi kumpa Daudi ufalme wa kifalme ambamo kupitia
kwake ahadi zilizotolewa kwa Ibrahimu na Israeli zitatimizwa kupitia ukoo wake.
Ni agano ambalo Mungu anaahidi mzao wa Daudi kutawala katika kiti cha enzi juu
ya watu wa Mungu. Kupitia agano hili nchi ya Israeli iliendelea kupanua mipaka
yake na kuwa taifa imara na lenye nguvu.
Agano hili linakuwa msingi wa
tumaini la Masihi na linaleta maana ya hangaiko la Injili kuonyesha Yesu
alikuwa Mfalme halali wa Wayahudi. Agano hili lilitimia pale Yesu Kristo, mzao
wa uzao wa Daudi, alipozaliwa katika Bethlehemu. Injili ya Mathayo inaanza kwa kuonyesha Kristo alikuwa “Mwana wa Daudi”
(Mt. 1:1), na hivyo alikuwa na haki ya kutawala watu wa Mungu. Petro alihubiri
kwamba Yesu Kristo alikuwa utimilifu wa ahadi ya Mungu kwa Daudi (Matendo
2:29-36).
Soma zaidi: 2 Sam 7; Zab 72,
89, na 132
Kwanini Maagano haya?
Wote ambao Mungu alifanya nao
agano walikua ni wawakilishi wa wanadamu wengine mbele za Mungu. Maagano haya
yalifanyika ili Mungu aweze kueneza na kuratibisha ufalme wake toka mbinguni
hadi duniani kupitia mwanadamu.
Agano la Mungu kati ya Adamu
na Nuhu (Mungu na Adamu/Mungu na Nuhu) yanatambulika kama maagano na ulimwengu
wote/mzima (universal covents – kwa lugha ya kiingereza), kwani maagano haya
yalihusisha wanadamu wote duniani. Adamu na Nuhu waliwawakilisha wanadamu wote
kuwa ni watu wa Mungu katika maagano haya. Na kama tunavyotambua, kila agano la
mungu lililotangulia liliendelea kuwa msingi wa agano lililofuata. Maagano yote
yaliyofuata yalijengwa juu ya maagano ya nyuma yake. Agano na Nuhu liliendelea
kujengwa juu ya Agano na Adamu, nk.
Agano la Mungu kati yake na
Abrahamu, Musa, na mfalme Daudi yanatambulika kama maagano ya kitaifa (national
covenants – kwa lugha ya kiingereza). Katika maagano haya wahusika waliwawakilisha
wana wa israel pamoja na wale walioingia katika taifa la israel kama wateule wa
Mungu. Mungu alichagua taifa la Israel kuwa chombo chake cha kueneza na
kuendesha ufalme wake hapa duniani.
Kwanini ni muhimu kwa mkristo kuyafahamu
maagano haya?
Kuyafahamu maagano haya ni
Muhimu kwa Mkristo kwasababu yanatuwezesha sisi kuona ni kwa jinsi gani hadithi
za Biblia zina umoja katika kudhihirisha ufalme wa Mungu na ahadi zake kwa mwanadamu,
hasa katika ahadi ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika dhambi na mateso. Pia
inatusaidi kuuona uaminifu wa Mungu toka kuwepo kwa misingi ya ulimwengu. Mungu
ni MUNGU wa maagano, ni Mungu mwaminifu, na ni Mungu ambaye hadi sasa hutimiza
maagano na ahadi zake kwetu sisi wanadamu.
Kama una swali au ushauri juu
ya Makala hii usisite kuwasiliana nami, nipo tayari kukusaidia kuelewa zaidi na
kujifunza juu ya ufalme wa Mungu. Pia kadri tunavyoendelea kujifunza
tutachambua maagano haya kwa kina zaidi kwa kuliangazia moja baada ya lingine
hapo baadae. Endelea kusoma blog hii kujifunza zaidi.
Kwasababu ya Kalvari mimi nimewekwa Huru,
Rumishael Ulomi
Copyright © www.kilicentric.com
Makala hii ipo kwa lugha ya KIINGEREZA HAPA
