Katika Makala iliyopita tulijifunza juu ya maagano ya Mungu
aliyofanya na mwanadamu ili kusimamia, kuratibu, na kueneza ufalme wake
duniani. Maagano haya yalikua ni yale yaliyofanyila katika Agalo la kale, kama haujafanikiwa
kuisoma Makala hii tafadhali BOFYA HAPAKUISOMA.
Tulijifunza kuwa, Agano la kwanza ambalo Mungu alifanya na
mwanadamu katika Biblia ni Agano alilolifanya na Adamu (Mwanzo 1-3, Hosea 6:7),
Hili lilikuwa ni agano la msingi kwa mwanadamu na lilikuwa ni msingi wa maagano
mengine yote yaliyofuata baadaye. Agano hili lilitoa malengo ya Ufalme wa Mungu
na wajibu na majukumu ya mwanadamu katika ufalme wa Mungu hapa duniani kabla na
baada ya mwanadamu kutenda dhambi na kwenda kinyume na Mungu. Katika Agano na
Adamu, mwanadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu ili kuratibisha shughuli na
kueneza ufalme wa Mungu ulimwenguni kote (Mwanzo 1:27-28, 5:1-2). Mungu aliumba
ulimwengu na wanadamu, akionyesha yeye ndiye mtawala mkuu wa wote na vyote
alivyoviumba. Aliwaumba Adamu na Hawa wakiwa makuhani-wafalme, kama wale
waliofanywa kwa mfano wake, wautawale ulimwengu kwa ajili ya Mungu. Walipaswa
kupanua utawala wa Mungu juu ya dunia yote.
Wapo wachache ambao husema kuwa Mungu hakufanya Agano na
Adamu na hii ni kutokana na kuwa Mungu hapo mwanzo hakutumia neno ‘Agano’
katika jambo lolote alilosema kuhusu Adamu. Lakini Tumshukuru Mungu kuwa
kupitia Nabii Hosea katika Hosea 6:7,
anatuelimisha juu ya hili na tunaamini kuwa Mungu alifanya Agano na Adamu.
Kutokuwepo kwa neno "agano", katika kumbukumbu za kibiblia hasa
katika kitabu cha Mwanzo haimaanishi kwamba hakuna agano lililokuwepo. Kupitia
Hosea tunajifunza kwamba Agano la kwanza ambalo Mungu aliwahi kufanya na
wanadamu lilikuwa ni Agano na mwanadamu wa kwanza, Adamu mwenyewe.
Wanatheolojia wanaliita agano hili ‘Agano la Mungu na Adamu’
kuwa ni agano la ‘kazi’ kwasababu linatokana na kanuni ya utii wa Adamu. Sehemu
ya kwanza ya Agano la Adamu ilikuwa na Baraka nyingi muhimu zilizoambata na
onyo kwa Adamu. Adamu na Hawa waliumbwa kwa mfano wa Mungu, na kupewa mamlaka
juu ya uumbaji wa Mungu, lakini kuna mambo ambayo walipaswa kutekeleza.
Mungu aliwabariki Adamu na Hawa kwa kuwaweka katika bustani
nzuri yenye malisho ya kila aina, katikati ya mito minne iliyojawa na maeneo
yenye kupendeza na kuvutia kuanzia miti mizuri hadi mawe ya thamani. Zaidi ya
yote Mungu aliwapa hadhi kubwa sana kwa kuwapa jukumu la kutawala uumbaji wake na
kuijaza dunia kwa uzawa wao. Mungu anawapa zawadi ya uhusiano na uwezo wa kuzaa
watoto na kuijaza dunia. Mungu alitoa mamlaka ya kuratibisha na kueneza ufalme
wake duniani kwa Adamu na Hawa. Mungu alikuwa aeneze ufalme wake duniani kupita
Adamu na Hawa.
Onyo ambalo Mungu alitoa kwa Adamu ni kuhakikisha kuwa
hawali tunda la mti wa mema na mabaya, kwani siku ambayo wangefanya hivyo
wangekufa (Mwanzo 2:17). Adamu alipaswa kumtii Mungu, na Mungu aliahidi uzima
wa milele kwa utii wa Adamu. Hivyo katika kupokea Baraka ya uzima wa milele,
kazi ya adamu ilikua ni kutii maagizo ya Mungu katika Agano hili.
Ni kwa masikitiko makubwa sana kuona kwamba pamoja na Adamu
kupewa maelekezo yote haya, bado Adamu alivunja Agano hili na Mungu alipochukua
tunda ambalo Hawa alimpa, na kulila, akikaidi amri ya Mungu na kuleta adhabu ya
kifo kwa wanadamu wote ulimwenguni (Warumi 5:12-14). Na kifo hakikuwa kwa
mwanadamu tu, bali hata kwa wanyama na mimea, na zaidi ya yote Adamu badala ya
kutubu na kurejea kwa Mungu alielekeza lawama zote kwa mkewe, na mkewe naye
akaelekeza lawama zote kwa yule nyoka (Mwanzo 3:12). Wakiufanya uumbaji wa
Mungu kuwa ndio chanzo cha anguko lao. Adamu
na Hawa walikuwa wametangaza uhuru wao kwa tendo moja la uasi dhidi ya Mungu. Walichokifanya
kilikuwa zaidi ya kula tu kipande cha tunda lililokatazwa. Kwa kiwango kikubwa,
walikuwa wamekaidi amri iliyo wazi ya Mungu. Walichagua kusikiliza sauti ya
kushawishi ya yule nyoka na kuruhusu kiburi chao wenyewe kuingia na kufanya
kazi. Walifanya kosa kubwa la kupinga waziwazi haki ya Mungu katika kuyaongoza
maisha yao, wakitumia mamlaka na uwezo juu ya maisha yao wenyewe.
Sehemu ya pili ya Agano hili tunaona jinsi Mungu
anavyoshughulika na kuvunjwa kwa Agano lake na mwanadamu. Hata pamoja na
mwanadamu kuanguka na Mungu kutoa adhabu ya kuwaondoa katika bustani ya Edeni,
tunaona Mungu mwenye huruma na upendo kwa mwanadamu aliyemuumba kwa mfano wake
mwenyewe akitoa ahadi nyingine ambayo itamrejesha mwanadamu katika uhusiano
mzuri na Mungu. Kutokana na dhambi ya Adamu ya kutokutii, daima kutakuwepo na
chuki kati ya Shetani na Hawa, na uzao wake. Mwanamke atazaa kwa uchungu, na
kutakuwa na kutokuelewana vizuri kati ya mwanamume na mwanamke. Udongo
utalaaniwa, miiba na michongoma itaonekana kwenye mimea, na kuishi kwa mwanadamu
kutakuwa kwa taabu na dhiki kwa ulimwengu wote wa asili (Warumi 8:22-23), na
mwishowe kifo kitakuwa hatima ya kila kiumbe hai (Mwanzo 3:14-19).
Licha ya hali ya kutisha ya laana hizi, na uharibifu
uliotokea, ndani ya laana na uharibifu huu palikuweno ahadi. Akizungumza na
Shetani, Mungu anasema “Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya
uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino”
(Mwanzo 3:15). Ni kweli kabisa kwamba mwanadamu humponda nyoka kichwa, na kugongwa
na nyoka juu ya kisigino chake, lakini laana hii haikukusudiwa kwa nyoka tu.
Ilinenwa kwa Shetani, kwa kutazamia ushindi wa Yesu Kristo katika kumkomboa
mwanadamu na kuleta uzima wa milele. Uzao wa mwanamke ni Yesu Kristo, ambaye
ingawa alichubuliwa na msalaba (Isaya 53:4-5), alimponda nyoka (Shetani) kichwa
(Wagalatia 4:4, 1 Yohana 3:8).
Umuhimu wa Agano hili
kwa Mkristo wa leo ni nini?
Ni vigumu sana kwa Mkristo kuelewa maana ya Agano jipya kama
hana maarifa ya kutosha juu ya Agano hili ambalo Mungu alilifanya na Adamu
bustanini Edeni, kwani kupitia Agano hili ndipo tunapoanza kuuona mpango wa
Mungu katika kuleta ukombozi/wokovu kwa mwanadamu baada ya kuanguka katika
dhambi. Hauwezi kuelewa sababu ya Kristo kufa msalabani endapo utakuwa umekosa
maarifa juu ya Agano hili.
Katika Agano hili, Mungu anaahidi kumpa Adamu uzima wa
milele ikiwa atamtii na kukataa kula tunda la mti uliokatazwa. Mungu alimwambia
Adamu kwamba ikiwa yeye na mke wake wangetii amri hiyo wangeishi milele.
Kupitia Agano hili tunaona kwamba baraka, uhisiano na Mungu, na uzima wa milele
zilitegemea utii au “kazi” ya Adamu na Hawa bustanini Edeni.
Agano hili la matendo kati ya Mungu na Adamu bado lipo, lakini
halina uwezo wa kuwaokoa wakosefu kwasababu halitoi msamaa wa dhambi wala uzima
wa milele, katika Agano hili sisi ni wenye dhami na wafu. Tangu hapo awali
baada ya kuanguka kwa mwanadamu katika dhambi hakuna mtu aliyeweza kushika
masharti ya agano la kazi kwa sababu sisi sote, bila ubaguzi, tumezaliwa katika
hatia ya dhambi ya kurithi ("dhambi ya asili"). Lakini kwao
walioamini katika Kristo kuna habari njema, kwani agano la matendo limetimizwa!
Yesu Kristo, Adamu wa Pili, alifanikiwa pale ambapo Adamu wa kwanza alishindwa.
Habari hizi tunazisoma katika kitabu cha Warumi 5:12–21,
ambapo mistari hii inasema kwamba Yesu, Adamu wa mwisho, alitupatia uzima wa
milele kwa utii Wake. Hivyo basi, ikiwa Adamu wa kwanza angalitii, yeye na
wazao wake hawangekufa kamwe, bali wangeishi milele. Lakini kwa kushindwa kwake
Adamu kutii, Kristo alitimiza agano hili kwa kutii kwake, na kupitia yeye mimi
na wewe tuna uzima wa milele, na tupo katika uhusiano mzuri na Baba yetu wa
Mbinguni. Na kama vile tulivyokufa katika dhambi ya Adamu, ndivyo tunavyoishi
sasa kwa sababu ya utii wa Mwana wa Mungu.
Adamu alishindwa kutii katika Agano la Kale, Lakini Kristo
alishinda katika Agano Jipya kwa kutii hadi kifo. Na kupitia yeye, kwa kutii
kwake, mimi na wewe tuna uzima wa milele. Adamu alikuwa mtu wa kwanza,
aliyeumbwa moja kwa moja na Mungu, kichwa cha mfano cha wanadamu. Yesu ndiye
Mungu-mtu wa kwanza, Mwana wa moja kwa moja wa Mungu, Kichwa cha Kanisa. Adamu
na Yesu waliingia ulimwenguni bila dhambi. Hata hivyo, ambapo Adamu alishindwa,
Yesu alishinda.
Adamu alitenda dhambi mara moja, na hivyo kuwaangamiza wanadamu.
Yesu alikufa mara moja, na hivyo kufunika wingi wa dhambi (Warumi 5:18-19).
Katika Agano la Mungu na Adamu tunajifunza kuwa, Mungu ni
Mungu mwenye Upendo na Rehema. Kutoka kizazi hadi kizazi upendo na Rehema za
Mungu kwetu zimeendelea kuonekana. Na tunajifunza pia kuwa, pamoja na madhaifu
yetu yote Mungu ameendelea kututafuta na kujenga uhusiano wake nasi. Kila
wakati Mungu ni Mwena, na Mungu ni mwema kila wakati.
Hatua gani tuchukue
ili kuendelea kukaa hemani mwa Bwana?
Adamu alipewa machagu mawili ‘Uzima wa milele au Kifo’, kwa
kukaidi kwake alichagua kifo na maisha yenye kujawa na taabu. Leo, baada ya
muda mrefu, Mungu anataka tuchague, tuchague uzima wa milele katika Kristo. Ni
kweli kwamba wanadamu wamepotoshwa na dhambi kiasi kwamba wanadamu hawamtafuti
Mungu peke yao (Warumi 3:11-12), lakini tunajunza pia kuwa Mungu ameendelea kupinga
matokeo haya ya dhambi kwa njia nyingi. (Matendo 10:34-35, Matendo 17:26-28,
Warumi 2:14-15) na kwamba sura ya Mungu katika wanadamu haijapotea kabisa (Mwanzo
9:6). Kwa hiyo, kwa neema ya Mungu, bado tunaweza kuchagua. Sambamba na agano
la Mungu na Adamu, injili ya Yesu Kristo inatuhimiza kufanya uchaguzi halisi
leo.
Mungu aliwahimiza wana wa Israel “wachague uzima”
(Kumbukumbu la Torati 30:19), Nasi tuchague uzima katika Kristo.
Kwasababu ya Kalvari mimi nimewekwa Huru,
Rumishael Ulomi
Copyright © www.kilicentric.com
Makala hii ipo kwa lugha ya KIINGEREZA HAPA
